TAARIFA ya mkaguzi wa ndani wa halmashauri ya wilaya ya Muleba imebaini kuwepo ubadhilifu wa zaidi ya milioni 231 zilizotumika kama malipo hewa kwa wakuu wa idara mbalimbali.
Katika taarifa yake mbele ya baraza la madiwani lililofanyika Jumamosi mkaguzi huyo Blasio Paul alisema ubadhilifu huo umefanyika katika kipindi cha robo ya tatu kwa wakuu wa idara kufanya udanganyifu kwenye akaunti za halmashauri.
“Posho kwa ajili ya shughuli nyingi zinazofanyika kwa wakati mmoja ni udanganyifu na matumizi mabaya ya fedha za halmashauri, kuna ubinafsi usio na maana unaofanywa na wakuu wa idara” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha taarifa hiyo inadai kuwa wakuu wa idara walilipwa posho wakati hawakuwa kwenye ukaguzi, kutokuwa nje ya vituo vya kazi kama walivyodai na kukiuka sheria za manunuzi ya umma namba 21 ya mwaka 2004.
Kufuatia ubadhilifu huo madiwani walijipanga kuwawajibisha watendaji waliotuhumiwa kwa ufisadi, juhudi ambazo zilizimwa na mkuu wa wilaya hiyo Angelina Mabula kwa kusoma barua ya Katibu Mkuu (TAMISEMI) kuwa hawaruhusiwi kumkataa mtendaji wa halmashauri.
Taarifa hiyo iliyosomwa na Katibu Tawala Erasimus Rutabanzibwa kwa niaba ya DC iliwafanya madiwani kuja juu na kikao hicho kuhairishwa kwa zaidi ya saa moja ambapo madiwani wa CCM walikutana kwa dharula.
Hatimaye baraza liliazimia kuitwa haraka kwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Mkuchika asikilize kilio cha madiwani na kutoa ufumbuzi wa tuhuma zinazowakabili watendaji walio chini ya wizara yake.
Mbunge wa Muleba Kasikazini Charles Mwijage (CCM) alijikuta matatani tena baada ya kutuhumiwa na madiwani kuwa alitoa kauli ya kutetea ufisadi huo, zikiwa ni siku tatu tangu apigwe mawe na kuzomewa na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Izigo.
Akimtuhumu mbunge huyo diwani wa kata ya Kamachumu Danstan Mutagaywa (CCM) alimtaka aeleze tafsili ya ubadhilifu wa fedha za wananchi kama sio taarifa iliyowasilishwa mbele yao na mkaguzi wa halmashauri hiyo.
Pia madiwani walidai mbunge huyo hakuonyesha msimamo wowote kuhusu hoja iliyokuwa mbele yao kutokana na kuwaunga mkono madiwani na wakati huo kuegemea upande wa watuhumiwa wa ubadhilifu.
Kikao hicho kiliendeshwa na Mwenyekiti wake George Katomelo na Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo Pastory Kajuna ambaye pia ni Ofisa elimu wa wilaya hiyo na mwandishi wa Fikra Pevu amepata nakala ya ripoti hiyo.
No comments:
Post a Comment