Katika kipindi cha miaka hamsini tangu tupate Uhuru yapo matukio mengi ya kihistoria ambayo yametokea katika mkoa wa Kagera. Mtiririko wa matukio hayo ni kama yanavyoainishwa hapa chini .
Mwaka 1961
• Uhuru wa Tanganyika : tarehe 09 Desemba 1961 Mkoa wa Kagera uliungana na mikoa mingine kusherehekea kupatikana kwa Uhuru. Sherehe hizo zilifanyika katika Uwanja wa Uhuru uliopo katika Manispaa ya Bukoba. Uwanja huo ulipewa jina hilo la Uhuru kwa kuwa ndio uliotumika kufanyia mikutano ya kisiasa katika harakati za kudai Uhuru. Maadhimisho makubwa yalifanyika kitaifa mkoani Dar es Salaamna mkoa uliwakilishwa na watu wanne ambao ni Ndugu Samweli Luangisa (Assistant Province Commissioner), Mzee Ziadi alikuwa Mwenyekiti wa TANU, ndugu Abdul Sued Kagasheki aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba na Ndugu Masabala aliwakilisha umoja wa vijana wa TANU.
Mwaka 1962
• Mafuriko : Mvua kubwa ilinyesha na mafuriko kutokea sehemu kubwa ya Mkoa, ambapo wananchi waliipa jina la “Mvua ya Uhuru” kwa sababu mvua kubwa ya masika ilinyesha baada ya Tanganyika kupata Uhuru.
Mwaka 1963
• TANICA Yaanzishwa : Kampuni ya Kukoboa Kahawa ya TANICA ilianzishwa. Kampuni hii imechangia kukua kwa pato la mwananchi wa mkoa wa Kagera. Tangu kuanzishwa kwake hadi sasa kampuni hii imetoa ajira nyingi sana kwa wakazi wa mkoa wa Kagera.
• Kufutwa kwa Tawala za Kichifu (Kitemi) : Tawala za kichifu za Ntare, Nyarubanja, Ruhinda na Rumanyika zilifutwa kutoka na serikali kufuta mfumo huo wa utawala kote nchini.
Mwaka 1965
• Kuanzishwa kwa Mkoa wa Kagera: Mkoa wa Ziwa Magharibi ambao sasa ni “Kagera” ulianzishwa.
• Uchaguzi Mkuu : Uchaguzi Mkuu ulifanyika ambapo ulihusisha watemi na Wakama. Watemi na Wakama waliotawala kuanzia mwaka 1965-1970 katika Mkoa wa Kagera ni wafuatao:
• Bakampenja - alitawala sehemu ya Ihangiro;
• Kaneno - aliongoza sehemu ya Karagwe;
• Kasusura – aliongoza sehemu ya Biharamulo;
• Kasano - aliongoza sehemu ya Kiziba na Missenyi;
• J. Kibogoyo – aliongoza sehemu ya Kiyanja; na
• Kami – aliongoza sehemu ya Bugabo na Kyamutwara.
Orodha ya Wabunge tangu Uhuru ipo kuanzia Kiambatanisho Na 4.
Mwaka 1966
• Ukame : Ukame mkubwa uliodumu hadi mwaka 1970 watokea na kusababisha njaa kali katika wilaya ya Karagwe. Hali hiyo ilisababisha baadhi ya watu kupoteza maisha, kupungua kwa nguvukazi, baadhi ya familia kukosa matunzo kwa ukaribu baada ya wanaume kwenda maeneo ya mbali kutafuta chakula.
Mwaka 1970
• Uchaguzi Mkuu : Uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge ulifanyika katika majimbo matano ya Uchaguzi ya Biharamulo, Bukoba, Karagwe, Muleba na Ngara. Waliochaguliwa kuwakilisha majimbo hayo ni Ndugu Kasusura (Biharamulo), Ndugu Ishungisa (Karagwe), Ndugu Zimbihire (Muleba) na Ndugu Niboye (Ngara). Kwa Wilaya ya Bukoba ambayo ilikuwa kubwa na ilikuwa ikiendeleza utawala wa watemi na wakama, iliwakilishwa na wawakilishi watatu kwa kupigiwa kura na wananchi wa Wilaya hiyo. Waliowakilisha wilaya hiyo walikuwa Ndugu Kibogoyo, Ndugu Kasano na Ndugu Rutagwerela.
Mwaka 1972
• Machafuko ya mpakani: Matatizo katika mpaka wa Tanzania na Uganda (Kaskazini mwa Mto Kagera) matatizo haya yalisababisha kutokea kwa vita ya muda mfupi kati ya Tanzania na Uganda ambayo baadaye tatizo hili lilimalizwa kwa suluhisho la nchi hizi mbili.
Mwaka 1975
• Kuanzishwa kwa Wilaya ya Muleba : Wilaya ya Muleba ilianzishwa kwa kuunganisha Tarafa ya Ihangiro, Kimwani na baadhi ya kata za Tarafa ya Kihanja.
Mwaka 1976
• Kuanzishwa kwa kijiji cha Kyamnyorwa katika wilaya ya Muleba kutokana na operesheni ya vijiji. Katika kijiji cha Kyamyorwa kulikua na ardhi yenye rutuba, na huduma nyingine muhimu kama maji. karibu na huduma stahili ambapo waliishi kwa pamoja na kufanya kazi kwa pamoja na miongoni mwa vijiji bora.
Mwaka 1977
• Kuanzishwa kwa Chama cha Mapinduzi : sherehe za kuzaliwa kwa chama cha mapinduzi zilifanyika mkaoni kwenye uwanja wa uhuru.
Mwaka 1978
• Vita kati ya Tanzania na Uganda : Mwezi Oktoba 1978 kulitokea vita kati ya nchi ya Tanzania na nchi ya Uganda . Vita hii ilijulikana kwa jina maarufu la “vita ya Kagera” iliitwa jina hilo kutokana kwamba ilipiganiwa katika ardhi ya Tanzania mkoani Kagera.
Vita hii ilisababishwa na kitendo cha Majeshi ya Uganda, chini ya Nduli Idd Amin Dada, kuvamia ardhi ya Tanzania katika eneo la Missenyi na kudai kuwa eneo lote lililo kaskazini mwa Mto Kagera ni ardhi ya nchi ya Uganda. Vita hivyo vilimalizika mwezi April, 1979 kwa Majeshi ya Tanzania kushinda vita na kumuondoa madarakani Nduli Idd Amin.
Vita hivi vya Kagera vilikuwa na athari kubwa kwa mkoa wa Kagera. Athari hizo ni pamoja na vifo, wananchi kunyang'anywa mali zao na uharibifu wa miundombinu ya majengo na barabara.
Mwaka 1979
• Mkoa wa Ziwa Magharibi wabadilishwa Jina : Baada ya vita kati ya Tanzania na Uganda Mkoa wa Ziwa Magharibi ( West Lake ) ulibadilishwa jina na kuitwa Kagera.
• Uwanja wa Uhuru wabadilishwa Jina: Uwanja wa Uhuru uliopo mjini Bukoba ambao ulitumika mwaka 1961 kusherehekea Uhuru ulibadilishwa jina na kuitwa “Uwanja wa Jenerali Mayunga” kwa kumbukumbu ya vita ya Kagera na heshima ya shujaa na kiongozi wa vita hivyo.
Mwaka 1983
• Operesheni Uhujumu Uchumi : Kutokana na kukosekana kwa bidhaa muhimu katika jamii na kupungua kwa uwianao wa kipato kati ya walio nacho na wasio nacho serikali iliendesha operesheni dhidi ya wahujumu uchumi nchi nzima. Wafanyabiashara wa Mkoa wa Kagera walitupa bidhaa zao kwenye Ziwa Victoria na mto Ngono ili kuhofia kukamatwa na Serikali.
• Kugunduliwa kwa Mgonjwa wa UKIMWI: Ugonjwa unadhoofisha kinga za mwili za kujikinga na maradhi, ambao baadae ulikuja kujulikana zaidi kama UKIMWI (Ukosefu wa Kinga Mwilini), uligundulika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania mkoani Kagera. Ugonjwa huu uligunduliwa katika hospitali ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ya Ndolage iliyoko wilaya ya Muleba ambapo mgojwa wa kwanza aliyegundulika kuwa na virusi vya UKIMWI alitoka katika Kijijini cha Kanyigo Wilaya ya Missenyi.Hospitali ya Ndolage ilikuwa ya kwanza kutoa huduma ya kupima UKIMWI katika mkoa wa Kagera.
Mwanzoni wananchi wa Mkoa wa Kagera waliuita ugonjwa huo “ Juliana” au “Slim”. Uliitwa Julianakwa sababu iliaminika kuwa ugonjwa huo uliingizwa nchini na vijana waliokuwa wakitokea Uganda wakiwa wamevaa mashati ya Juliana. Pia uliitwa ‘slim' kwa sababu waathirika wa ugonjwa huo walikuwa wanakonda hadi kufa. Ugonjwa huu baadae ulienea Tanzania nzima na kuleta athari kubwa katika jamii. Mkoa wa Kagera ulikuwa wa kwanza kuathirika. Ugonjwa huu uliwakumba zaidi vijana, wanajamii ambao wanaotegemewa sana katika uzalishaji mali . Vijana wengi wakaangamia kwa UKIMWI na kufanya familia nyingi kubaki na wazee wakibeba mzigo wa kutunza watoto yatima. Pia muda mwingi wa kuzalisha mali ulipotea katika kuhudhuria mazishi na matanga ya ndugu na jamaa, kuuguza wagonjwa na kutunza yatima. Ugonjwa wa UKIMWI bado upo mpaka sasa katika mkoa wa Kagera na Tanzania kwa ujumla ambapo kiwango cha maambukizi mkoani Kagera ni asilimia 3.4.
Mwaka 1985
• Uchaguzi Mkuu: Uchaguzi ulifanyika kwa amani na utulivu, na Tanzania ilipata Rais wa awamu ya pili Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi.
Mwaka 1990
• KDCU na KCU Vyaanzishwa: Chama Kikuu cha Ushirika cha Wilaya ya Karagwe na Chama Kikuu cha Ushirika cha Kagera (KCU) vyaanishwa.
Mwaka 1992
• Mfumo wa Vyama Vingi: Mfumo wa vyama vingi vya siasa waanzishwa nchini na kuingia mkoani Kagera kwa kufunguliwa matawi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), United Democratic Party (UDP), NCCR-Mageuzi, United Movement for Democracy (UMD) na Tanzania Labour Party (TLP).
Mwaka 1994
• Kuingia kwa Wakimbizi wa Rwanda na Burundi : Kutokana na mapigano ya kikabila nchini Burundi na mauaji ya kimbari nchini Rwanda , inakadiriwa kuwa Wanyarandwa na Warundi 750,000 waliingia mkoani Kagera wakikimbia mapigano hayo. Ujio wa wakimbizi ulisababisha madhara makubwa kwa mkoa wa Kagera yakiwemo uharibifu wa mazingira na kushamili kwa uhalifu mwingiliano wa utamaduni, kuzaliana Hadi kufikia Juni, 2011 wakimbizi wote walikuwa wamerudi katika nchi zao.
• Kuanguka kwa ndege: Ajali ya kuanguka kwa ndege ya Jeshi yasababisha vifo na majeruhi kwa abiria waliokuwemo ndani ya ndege hiyo
Mwaka 1995
• Mvua kubwa: Mvua kubwa ilinyesha na kusababisha mafuriko na uharibifu wa mazao na miundombinu. Mafuriko yaliathiri sana Wilaya yote ya Bukoba na Missenyi. Madaraja yalisombwa na maji hivyo kuathiri watumiaji na baadhi ya nyumba za watu ziliharibiwa.
• Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa Vyama Vingi : Kutokana na kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 uchaguzi mkuu ulifanyika ukihusisha vyma vingi. V yama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi huo mkoani Kagera ni Chama cha Mapinduzi (CCM), United Democratic Party (UDP), NCCR-Mageuzi, United Movement for Democracy (UMD) na Tanzania Labour Party (TLP).
Mwaka 1996
• Kuzama kwa MV Bukoba: MV Bukoba ikiwa safirini kutoka Bukoba kwenda Mwanza, ilizama katika Ziwa Victoria kilomita nane kabla ya kufika bandari ya Mwanza. Inakadiriwa kuwa watu mia nane (800, kati yao watu wapatao 580 wakikadiriwa kutoka Mkoa wa Kagera). Aidha mali yenye thamani ya mamilioni ya shilingi ilipotea. Sababu za kuzama kwa meli hiyo kulisababishwa na ujazaji wa abiria na miziko kupita uwezo wake.
Kiasi cha shilingi 294.4 kilitolewa na Serikali kwa Mkoa wa Kagera, ikiwa ni rambirambi kwa wafiwa na pole kwa walionusurika.
Mwaka 1997
• Mradi wa KAEMP waanzishwa: Katika kukabiliana na athari za wakimbizi, mkoani Kagera mradi mkubwa wa Kilimo na Usimamizi wa Mazingira, uliojukana zaidi kwa jina la KAEMP ( Kagera Agricultural and Environmental Management Program ) ulianzishwa. Programu hii ilileta mapinduzi makubwa katika maendeleo ya kilimo, mazingira, afya, maji na barabara.
• Mvua za El – Nino: Mvua kubwa za El Nino zilinyesha na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu ya wakazi wa Kagera hasa barabara na madaraja. Aidha, nyumba na mali mbalimbali za wananchi ziliharibiwa hivyo wananchi kuhitaji msaada wa Serikali.
Mwaka 2000
• Uchaguzi Mkuu : Uchaguzi mkuu wa pili katika mfumo wa vyama vingi wafanyika huku kukiwa na ongezeko la majimbo ya uchaguzi. Majimbo hayo mapya yalitokana na kugawanywa kwa Jimbo la Muleba na kuwa na majimbo ya Muleba Kaskazini na Muleba Kusini na kugawanywa ka Jimbo la Biharamulo na majimbo ya Biharamulo Mashariki na Biharamulo Magharibi. Jimbo la Bukoba pia liligawanywa na kuwa na majimbo ya Bukoba Mjini, Bukoba Vijijini na Nkenge. Jimbo la Karagwe nalo liligawanywa na kuwa majimbo ya Karagwe na Kyerwa.
Mwaka 2002
• Benki ya Wakulima (KFCB) Yaanzishwa: Benki ya wakulima ambayo inamilikiwa na kusimamiwa na vyama vya ushirika vya msingi, vyama vya ushirika vya kuweka na kukopa, mfuko wa mazao na chama kikuu cha ushirika KCU ilianzishwa. Makao makuu ya benki hii yapo Manispaa ya Bukoba
• Oparesheni maalum ya kusaka majambazi: Oparasheni hii ilihusisha vikosi mbalimbali vya Jeshi kutoka Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Mgambo pamoja na Idara ya Usalama wa Taifa. Idara ya Wanyamapori nayo ilihusika katika zoezi hili. Kwa ujumla zoezi hili lilikuwa na mafanikio makubwa
Mwaka 2004
• Kuwashwa kwa Mwenge wa Uhuru: Mwenge wa Uhuru wawashwa kwenye uwanja wa Kaitaba na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Ali Mohamed Shein tarehe 07 Juni 2004 na kukimbizwa katika Wilaya zote za mkoa wa Kagera na baadaye kukabidhiwa Mkoa wa Kigoma.
Mwaka 2006
• Kuanzishwa kwa Wilaya ya Chato: Wilaya ya Chato yaanzishwa kwa kuigawa Wilaya ya Biharamulo. Eneo la wilaya mpya ya Chato ni eneo lote la liliokuwa Jimbo la Uchaguzi la Biharamulo Mashariki likiwa na Tarafa 3, Kata 14 na Vijiji 74. Bw. Said Mkumbo ndiye alikuwa mkuu wa wilaya wa kwanza wa wilaya hiyo.
• Kuanzishwa kwa Wilaya ya Missenyi: Wilaya ya Missenyi yaanzishwa kwa kuigawa Wilaya ya Bukoba. Wilaya ya Missenyi ina ukubwa wa hekta 270,875, na inaundwa na tarafa 2, kata 20, vijiji 74 na vitongoji 350. Ina jimbo moja la uchaguzi liitwalo Nkenge, madiwani 20 wa kuchaguliwa na 8 viti maalum. Bw. Elias Maarugu ndiye alikuwa mkuu wa wilaya wa kwanza wa wilaya hiyo.
Mwaka 2007
• Kagera Day : Kagera Day Fund Rising” ilifanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee tarehe 27 Novemba 2007 ili kuchangisha fedha kwa ajili ya maendeleo ya elimu mkoani Kagera. Mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu, ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Fedha zilizopatikana zilisaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa na maabara na ununuzi wa bati. Madarasa matatu yalijengwe katika shule ya sekondari za Ijuganyondo (mjini Bukoba) na madarasa matatu pia katika shule ya Sekondari Bugene (iliyopo wilayani Karagwe).
Aidha, maabara yalijengwa katika shule sita za Kagondo (Muleba), Shyunga (Ngara), Rubondo (Biharamulo), Makurugusi (Chato), Izimbya (Bukoba Vijijini) na Bunazi (Missenyi).
Jumla ya bati 600 zilinunuliwa na kugawanywa bati 75 kwa kila Halmashauri.
Mfuko wa Kagera Day umeweza pia kupata wafadhili ambao wameleta kompyuta 51 kwa ajili ya wanafunzi wa shule za sekondari.
Mwaka 2009
• Mafuriko Chato: Mvua kubwa yanyesha wilayani Chato na kusababisha mafuriko makubwa yaliyoharibu mazao mashambani na miundombinu mbalimbali.
No comments:
Post a Comment